Nigeria mabingwa wapya Afrika 2013,yailaza Burkina Faso 1-0 katika mchezo wa fainali nchini Afrika Kusini.
Ni shangwe na vigelegele katika miji mbalimbali
nchini Nigeria baada ya timu yao ya The Super Eagles, kuibuka mabingwa
wapya wa Kombe la Mataifa ya Afrika.Mbio za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika zilizoanza tarehe 19 Januari zimehitimishwa, Jumapili, tarehe 10 Februari kwa Nigeria kuibuka bingwa wa fainali za mwaka 2013 barani Afrika.
Bao la mchezaji Sunday Mba alilofunga katika dakika ya 40 ya kipindi cha kwanza cha mchezo mjini Johannesburg, ndilo lililowahakikishia The Super Eagles, Nigeria kuwa mabingwa wapya.
Mchezo huo ulianza kwa kasi, timu zote mbili zikishambuliana kwa zamu. Hata hivyo Nigeria ndiyo walionekana kutawala zaidi mpambano huo na kukosa magoli kadha ambayo yangeipa ushindi mnono Nigeria.
Emmanuel Emenike aliibuka mfungaji bora wa mashindano hayo na kupata kikombe, huku Moses Victor akiwa mchezaji bora wa mechi kati ya Nigeria na Burkina Faso.
Mechi hiyo ya fainali ilihudhuriwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, akiwa mgeni rasmi, akiambatana na rais wa Fifa Sepp Blatter na rais wa CAF, Issa Hayatou.
The Super Eagles pia waliahidiwa zawadi kem kem, zikiwemo fedha taslim kwa kocha na wachezaji, hata kabla ya kutwaa ubingwa.
Hii ni zawadi kubwa kwa kocha wa Super Eagles, Stephen Keshi ambaye mwaka 1994, wakati Nigeria ilipotwaa ubingwa wa Afrika, alikuwa nahodha wa timu hiyo katika fainali zilifanyika nchini Tunisia.
Pia Nigeria ilitwaa ubingwa mwaka 1980, wakati fainali hizo zilipoandaliwa nchini Nigeria.
Super Eagles kama ilivyo kwa timu nyingine barani Afrika, itakuwa ikijiandaa kikamilifu kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwaka 2014.
0 comments:
Post a Comment