UTANGULizi
-
Amesoma S/Msingi Mbuyuni (Dar) | Alichaguliwa kwenda Ilboru lakini
hakwenda, akaenda Maua Seminary na alipata A tisa | Alisoma A-Level Tambaza | Ana BBA toka UDSM
- Amtaka Ridhiwan aongee na 'mshua' juu ya tatizo la maji Dar!
Nilikuwa
katikati ya kazi jimboni nikaambiwa kwamba kuna mwito humu wa Nape na
Ridhwan kutaka nieleze elimu yangu. WanaCCM walianza suala hili kwa ari,
nguvu na kasi mpya niliposema kwamba nchi imefika hapa ilipo kwa sababu
ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM.Nikapuuza,
naona sasa limeibuka tena kwa ari, nguvu na kasi zaidi baada ya
yaliyojiri bungeni kuhusu hoja binafsi niliyowasilisha bungeni kuhusu
maji na mkutano wa hadhara wa tarehe 10 Februari 2013 na masuala ambayo
niliipa Serikali wiki mbili kuyatolea majibu ama sivyo nitaongoza
maandamano ya wananchi kwenda Wizara ya Maji kutaka uwajibikaji na hatua
za haraka.Kwa mara nyingine tena
zinafanyika jitihada za kuhamisha wananchi kwenye mjadala kwa
kumshambulia mtoa hoja badala ya hoja, sasa ili turejee kwenye mijadala
ya msingi ni muhimu niweke kumbukumbu sawa kuhusu masuala kadhaa kama
yalivyoombwa.Elimu yangu sio
siri, nimegombea ubunge mara mbili mwaka 2005 na 2010 na mara zote
nimeeleza kuhusu suala hili; Nape na Ridhwan wangetumia tu elimu yao
wangetafuta kwenye mitandao na kukuta majibu wanayoyatafuta. Nieleze
kwa muktasari tu; nimesoma shule ya msingi Mbuyuni Dar Es Salaam
(nilikuwa mwanafunzi wa kwanza kwa mkoa wa Dar es Salaam).
Nilichaguliwa
kwenda Shule ya Sekondari ya Ilboru wakati huo ikiwa ya vipaji maalum,
sikwenda; wito ulinituma kwenda Seminarini. Nilisoma Franciscan Seminary
Maua (FRASEMA) mpaka kidato cha nne; nilipata daraja la kwanza; nikiwa
na alama A katika masomo tisa.Ningeweza
kwenda shule yoyote ya Serikali ya kidato cha tano na sita yenye
mchepeo ambapo ningeutaka; lakini niliamua kubaki Dar es Salaam shule ya
Tambaza kwa sababu nilitaka kusoma huku nikiendelea na harakati ambazo
nilizianza kabla.Hapa ndio
ilikuwa chanzo cha mimi kuingia kwenye kazi ya kuhamasisha mabadiliko
kwenye mimbari nje ya utumishi wa madhabahuni. Tukio lililobadili
mwelekeo wa maisha yangu, mwaka 1998 nikiwa kidato cha nne; nimesoma na
tumeanza mitihani tukatangaziwa kwamba mitahani yote imefutwa baada ya
kuvujishwa.Tukarudishwa nyumbani
kipindi hicho nikaenda kwenye mafungo kujitafakari kwenye mkoa mmoja
nikarejea Dar es Salaam nikakutana na wanaharakati kadhaa wa asasi
zisizo za kiserikali; maelezo kuhusu ufisadi yalinifanya nione nina
wajibu kwa nchi yangu, nikarejea Seminarini kufanya mitihani nikiwa na
fikra tofauti.Matokeo yakatoka
nimefanya vizuri, kwa mifumo yetu mibovu ya wakati huo kwa mara ya pili
tena Serikali hii inayoongozwa na CCM haikutambua vipaji na nikapaswa
niendelee kujilipia ada mwenyewe kama ilivyokuwa kwa ngazi nyingine za
elimu zilizotangulia; hapa nikakata shauri kwamba nitatumia uwezo na
uadilifu wote ambao Mwenyezi Mungu amenijalia kuwezesha mabadiliko
katika taifa letu.Nikaamua kuacha
kwenda kwenye shule za bweni mikoani na kubaki Dar es salaam nisome
Tambaza huku nikiendelea na kazi za harakati; wakati huo nikihamasisha
masuala ya ukombozi wa vijana nchini.Pamoja na kusoma kutwa huku nikifanya kazi nilipata daraja la pili katika kidato cha sita.
Taasisi
nilizoanzisha au nilizoongoza katika kipindi hicho na kazi nilizofanya
sio siri na zinapaswa kujieleza zenyewe kwa matendo badala ya maneno. Katika
kipindi hicho, wakati huo kukiwa hakuna Mfuko wa Elimu wala Bodi ya
Mikopo nikashiriki katika ushawishi wa mabadiliko ya kimfumo; nilikwenda
Dodoma, tukakutana na wabunge na mawaziri nikawasilisha mada “Towards a
more functional education in Tanzania”, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa
Sekondari.Kati ya wabunge
waliosikiliza mada niliyoiwaisilisha wakati huo sasa ni Rais Jakaya
Kikwete ( Ridhwan ukiwa nyumbani unaweza kumwuliza maoni yake aliyotoa
siku hiyo kuhusu ugharamiaji wa elimu na suala la mauaji ya mwanafunzi
wa Iyunga Michael Sikupya). Nilipotoka kwenye mkutano ule Dodoma
mwishoni wa miaka ya tisini, nilikata shauri kwamba mwaka 2005
nitagombea Ubunge hii ni baada ya kushudia aina ya wabunge waliokuwepo.Mwaka
2002 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Es Salaam kusomea “Bachelor in
Business Administration (BBA) kwenye programu ya jioni; nilifanya hivyo
kwa kuamua kwa kuwa nilitaka nisome huku nikiendelea na kazi. Mkuu
wa Programu hiyo wakati huo alishangaa sana kwa umri wangu (wakati huo
shahada hiyo walikuwa wakisoma wazee watu wazima wafanyakazi) na matokeo
yangu (kwa kuwa yaliniruhusu kwenda kuingia kusoma katika mfumo wa
kawaida). Nikamweleza akanielewa kwamba sitaki kusoma kama wanachuo
wengine wa kawaida, uamuzi wangu huo ulikuwa na gharama kwa kuwatafsiri
yake ni kuwa nilipaswa kujisomesha binafsi.Kwa
hiyo mimi ni kati ya wale ambao hatudaiwi na nchi hii kwa maana ya
kwamba sijawahi kuchukua ruzuku wala kusomeshwa na Serikali hii
inayoongozwa na CCM; nimesoma kwa jasho la wazazi wangu na langu
binafsi. Kwa hiyo, nijibu tu kuhusu
elimu yangu ya juu kwamba nimesoma miaka mitatu Chuo Kikuu cha Dar Es
Salaam (mtu aliyosoma kwa kiwango hicho kwenye baadhi ya vyuo duniani
hupewa associate degree).
Mwaka 2004 ikaanza misukosuko
mbalimbali, mwaka huo ulikuwa ndio unatungwa muswada wa Sheria ya Bodi
ya Mikopo ya Elimu ya Juu, haya matatizo yanayotokea leo niliyatabiri
wakati huo.Niliwasilisha mada kwa
wanachuo kwenye ukumbi wa Nkurumah kuchambua udhaifu wa muswada huo na
kupata maoni ya wanafunzi kuhusu marekebisho yanayohitajika; wanachuo
wakapitisha azimio la kwamba muswada huo upingwe.Kesho
yake nikiwa Morogoro kikazi kukafanyika mgomo hatimaye wanafunzi
wakapigwa na kukamatwa.Nakumbuka nilikatiza kazi niliyokuwa nafanya
nikarejea kwa kuwa Chuo kiliweka sharti kwamba lazima wanachuo waache
mgomo ndio waliokamatwa waachiwe. Wakati huo Serikali ya wanafunzi
ilikuwa haisikilizwi, mimi na wengine wachache tukajitolea kuzunguka
kampasi na hosteli zote kushawishi wanafunzi kurejea masomoni na
wakafanya hivyo.Serikali ya CCM
ikatoa maelekezo kwamba kama tumeweza kuwafanya wanafunzi warudi, hata
kama sikushiriki mgomo na sihusiki na masuala ya mikopo kwa kuwa ni
mwanafunzi ninayejilipia mwenyewe lazima nisimamishwe; nikiwa mwanafunzi
pekee wa BBA niliyesimamishwa wakati huo.Nikarejea
baada ya muda tayari kukiwa na mvutano kati yangu na utawala, mwaka
2005 nikaamua kugombea Ubunge wakati huo nikiwa mwanafunzi; mvutano
ukaongezeka zaidi. Na utawala wa Chuo ukawa unapata mashinikizo mengi
kutoka kwa Serikali na CCM; wengine wakipendekeza nifukuzwe, wengine
nifelishwe na wengine nisiruhusiwe kuingia katika maeneo ya Chuo jioni
masomoni kwa kuwa nitakuwa nafanya kampeni.Nikawa
katika mtanziko(dilemma) wa kuchagua ama kuendelea na masomo na kujitoa
au kupunguza nguvu kwenye kampeni (mbinu nyingi zilitumika wakati huo,
sio sehemu ya majibu yangu ya leo) au niendelee na kampeni. Nafsi yangu
ikanituma kuamua kuandika barua yakuahirisha masomo, baada ya matokeo ya
uchaguzi wa mwaka 2005 mazingira yalikuwa yamebadilika sana kuweza
kurejea kumalizia mwaka au miezi michache iliyokuwa imebaki.Mwaka
2006 nikiwa Marekani nilitafakari sana na kufikia uamuzi wa kuendelea
na kazi hii ya kusimamia mabadiliko na kujiandaa na uchaguzi wa mwaka
2010. Mwaka 2010 niligombea tena na kushinda wakati huo huo nikiongoza
kazi za kitaifa za kampeni makao makuu pamoja na Profesa Baregu na
wengine; hakuna mahali popote nilipowadanganya wananchi kuhusu elimu
yangu, kama nilivyoeleza hapo juu.
Naamini wananchi wa Jimbo la
Ubungo walinichagua kwa uwezo na uadilifu wangu, na walijua pia kwamba
nilikuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa miaka mitatu. Naamini
elimu ni kitu muhimu sana kwa kiongozi, lakini wapo wenye elimu kubwa
ya vyeti lakini hawajaelimika na wapo wenye elimu ndogo sana ya vyeti
lakini wanaelewa mkubwa wa kutimiza majukumu yao ya uongozi.Tangu
mwaka 2012 na 2013, nimekuwa kwenye mtanziko mwingine na viongozi wangu
ndani ya chama wanafahamu; niliomba kuachia majukumu mengine yote
katika chama ili nibaki na ubunge peke yake niweze kuwatumikia wananchi
wakati huo huo niendelee na masomo zaidi ya elimu ya juu katika fani
inayoendana na kazi ninayoifanya ya sasa na matarajio yangu ya baadaye.Hata
hivyo, kwa mwelekeo huu wa Serikali na CCM leo nieleze tu kwamba
nikifanya hivyo itakuwa faida zaidi kwa watawala tunapoelekea mwaka
2015; hivyo, nimeamua kama nilivyoamua mwaka 2005; kwamba nitarejea
masomoni baada ya CCM kuondoka madarakani na Tanzania kupata Serikali
mpya itakayoongozwa na CHADEMA. Kwa sasa nitaendelea kujisomea kila siku
ninapopata wasaa kwa kuwa elimu haina mwisho.Wakili
Ridhwan katika maandiko yake amefanya rejea ya suala Kihiyo wa CCM
Temeke, nashauri arejee kwenye hukumu ya kesi ile na marekebisho ya
sheria yaliyofanywa na Serikali yaCCM kuwalinda wabunge wake vihiyo
baada ya hukumu.
Mifano hailingani kwa sababu mimi sijatoa
maelezo ya uongo popote. Lakini hata kwa wabunge wa CCM wanaotoa maelezo
ya uongo wa wapiga kura, marekebisho hayo yamewawekea wigo wa mianya
yakutokea mahakamani.
Zamani
fomu zakuogembea zilikuwa na mahali pa kujaza elimu ya mgombea, sasa
kipengele hicho kimeondolewa. Hivyo, suala la kughushi na kutoa taarifa
za uongo haliko kama ilivyokuwa awali, isipokuwa kesi inaweza
kufunguliwa ya ukiukwaji wa kawaida wataratibu za kampeni kwa
kuwashawishi wapiga kura kwa taarifa za uongo (ndani ya ule muda wa
kisheria wa kesi kufunguliwa ambao ulishapita).
Halafu ni jukumu
la mlalamikaji sio tu kuthibitisha kwamba uongo ulitolewa bali uongo
umeathiri vipi matokeo. Ndio maana leo kuna vihiyo wengi tu wa CCM ndani
ya Bunge lakini ni vigumu kuwabana kwa mfumo wetu wa sasa.
Baada
ya majibu hayo marefu, naamini sasa Nape unaweza sasa kurejea kwenye
kujibu; Elimu ya Mnyika ina uhusiano gani na CCM kuahidi kwenye ilani
yake na kushindwa kutekeleza kwamba ifikapo mwaka 2010 asilimia 90 ya
wananchi wa mijini ikiwemo Dar essalaam watakuwa wanapata maji safi na
salama? Ridhwan kwa kuwa umeweza kufanya rejea unaweza pia kueleza ni
kwanini Rais Kikwete mwaka 2011 aliahidi kuwa tatizo la maji Dar es
Salaam litakuwa historia mwezi Februari 2013 lakini mwezi huo umefika na
matatizo bado ni makubwa?
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment